Haya tujenge
_Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema. Nehemia 2:18._
✍🏻 Moyo wake ukiwa umeumizwa kwa huzuni, mgeni kutokea mbali alitazama kingo zilizoharibiwa za Yerusalemu aliyoipenda. Je, sivyo malaika wa mbinguni wanavyotazama hali ya kanisa la Kristo? Kama wakazi wa Yerusalemu, tunazoea uovu uliopo na mara kwa mara tunaridhika huku tukikaa bila kufanya jitihada yoyote ya kuuondoa. Lakini maovu haya yanaonwaje na wale ambao wameangaziwa na Mungu? Je, hawaangalii kuta zilizoharibiwa na malango yaliyochomwa moto kwa mioyo iliyojaa huzuni kama Nehemia alivyokuwa?
✍🏻 Nehemia alibeba utume wa kifalme uliohitaji wakazi washirikiane naye katika kujenga tena kuta za mji, lakini hakutegemea matumizi ya mamlaka. Badala yake alitafuta imani na kukubaliana na watu, hali akijua kwamba muunganiko wa mioyo pamoja na mikono vilikuwa ni muhimu katika kazi kuu iliyokuwa mbele yake.
✍🏻 Lipo hitaji la wakina Nehemia kanisani leo, -- sio watu watakaoomba na kuhubiri tu, lakini watu ambao sala na mahubiri yao yanaungwa mkono na kusudi thabiti na ari…. Mafanikio yaliyopelekana na jitihada za Nehemia yanaonesha kile ambacho maombi, imani na hekima, matendo ya nguvu yatakamilisha…. Ile roho inayodhihirishwa na kiongozi, kwa kiasi kikubwa itaakisiwa na watu. Ikiwa viongozi wanaodai kuamini ukweli mtakatifu, wa muhimu ambao utakuwa ni jaribio kwa ulimwengu wakati huu, hawataonesha shauku ya dhati ya kuwaandaa watu kusimama katika siku ya Mungu, ni lazima tutarajie kanisa kuwa zembe, vivu na lenye kupenda anasa.
✍🏻 Nehemia alikuwa mwana matengenezo, mtu mkuu aliyeinuliwa kwa ajili ya wakati wa muhimu. Alipokutana na uovu na kila namna ya upinzani, ujasiri mpya na shauku viliamshwa. Nguvu na azma yake vilitia moyo watu wa Yerusalemu; na nguvu na ujasiri vikachukua nafasi ya unyonge na kukata tamaa. Kusudi lake takatifu, tumaini lake kuu, kujitoa kwake kwa furaha kwa ajili ya kazi, viliambukiza. Watu walinasa shauku ya kiongozi wao na katika eneo lake kila mtu akawa Nehemia na akasaidia kuimarisha mkono na moyo wa jirani yake.
*UBARIKIWE NA TAFAKARI NJEMA*
Comments
Post a Comment